Brazzaville: Tarehe ya kura ya maoni itakuwa 25 Okt
Serikali ya Kongo-Brazzaville imetangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ya nchi hiyo. Kwa mujibu taarifa hiyo, kura hiyo ya maoni ambayo imeibua makelele mengi nchini humo, itafanyika tarehe 25 mwezi huu wa Oktoba. Baraza la Mawaziri limesisitiza kuwa, ikiwa kura hiyo ya maoni itapitishwa, basi kutazaliwa taifa jipya kabisa nchini Kongo-Brazzaville. Katika katiba hiyo mpya, kipindi cha rais kusalia madarakani kimepunguzwa kutoka miaka saba na kufikia mitano, huku umri wa chini kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo ukipunguzwa pia kutoka miaka 40 na kufikia 30. Aidha kipengee cha kutopindukia umri wa miaka 70 kwa mtu anayetaka kugombea nafasi ya uraisi, ambacho kilipitishwa mnamo mwaka 2002, nacho kimefutiliwa mbali. Rais Denis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 72, amekuwa madarakani nchini humo kwa miaka 30 sasa, na ikiwa katiba mpya itapitishwa basi atakuwa na nafasi ya kugombea tena katika uchaguzi ujao. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Kongo-Brazzaville rais anatakiwa kuondoka madarakani kwa kumalizika mihula miwili ya uongozi. Wapinzani wanamtuhumu Rais Sassou Nguesso kuwa anafanya njama ya kumsafishia njia ya kuendelea kusalia zaidi madarakani.
chanzo-tehran radio
Post A Comment
Hakuna maoni :