technology

Watu 61 wameuawa katika machafuko mapya CAR


Watu 61 wameripotiwa kuuawa katika machafuko ya wiki kadhaa zilizopita nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jana viongozi wa nchi hiyo walitangaza kuwa, machafuko hayo yaliyoibuka mwishoni mwa mwezi Septemba uliopita, mbali na watu 61 kuuawa, zaidi ya wengine 300 walijeruhiwa. 

Kabla ya hapo takwimu zilizotolewa na Wizara ya Usalama wa Jamii zilionyesha idadi ya watu waliouawa katika machafuko ni 40, hata hivyo idadi hiyo imepanda na kufikia 61. 

Wizara ya Usalama wa Jamii imesisitiza kuwa, machafuko hayo ya hivi karibuni ni makubwa zaidi kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Serikali ya mpito ya Bangui imetajwa kuwa chanzo cha machafuko hayo na kwamba yalizushwa kwa lengo la kutaka kuahirisha uchaguzi mkuu ujao. 

Machafuko hayo yaliibuka baada ya kuokotwa katika jalala mwili wa kijana wa Kiislamu aliyekutwa amekatwa kichwa na watu wasiojulikana. Hii ni katika hali ambayo taasisi za kiraia mjini Bangui, zimejikuta katika hali ngumu ambapo zimeshindwa kuendelea na shughuli zake za kawaida. Taarifa iliyotolewa na mashirika hayo imesema kuwa, katika machafuko hayo ofisi zao kadhaa zilishambuliwa na kuporwa nyaraka muhimu na kung’olewa milango na madirisha suala ambalo limekwamisha kabisa shughuli zao.
chanzo-tehran radio
Post A Comment
  • Blogger Comment using Blogger
  • Facebook Comment using Facebook
  • Disqus Comment using Disqus

Hakuna maoni :