Habre azua kihoja mahakamani
Kiongozi huyo alishikwa na walinzi alipomfokea hakimu pale upande wa mashtaka ulipoanza kusoma orodha ya majina ya watu waliouawa ama kupotea wakati wa utawala wake.
Bwana Habre anatuhumiwa kwa kuamrisha mauaji ya watu 40,000 wakati wa utawala wake mnamo miaka ya 80.
Kesi hiyo ilihairishwa mwezi Julai baada ya bwana Habre kupinga mahakama hiyo akiitaja kuwa isiyo halali ambapo pia aliwashauri mawakili wake wasihudhurie.
Mahakama baadaye ilimpa mawakili ambao waliomba takriban siku 45 iliwajifahamishe yanayojiri katika kesi hiyo.
Siku 45 baadaye mawakili watatu walioteuliwa wamepata muda wa kutosha kuiangalia kesi hiyo lakini mteja wao hawatambui na amekataa kuwasiliana nao.
Jaji wa mahakama ya Burkinabe, Gberdao Gustave Kam ataamua iwapo kesi hiyo itaendelea bila upande wa utetezi wa Hissene Habre.
Tangu mwanzo wa utaratibu wa kesi hiyo, Hissene Habre, mwenye umri wa miaka 72, amekuwa akikataa kutambua uhalali wa mahakama maalum ya Afrika, ambayo iliundwa na Umoja wa Afrika mwaka 2013, ili kushugulikia kesi yake nchini Senegal.
Rais huyo wa zamani wa Chad hajawahi kujibu maswali ya jaji.
Kucheleweshwa kwa kesi hiyo kwa siku 45 kutaongeza bajeti kwa asilimia tisini.
Kesi hiyo ilikadiriwa kuchukua muda wa siku 90 pekee.
Waathirika ambao walifanya kampeni ya miaka 25 kuhakikisha ameshtakiwa wanatarajia kuwa mahakama hiyo itatenda haki.
Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo maalum atajaribu kuwasilisha ushahidi kuonyesha kuwa Habre aliamuru mauaji na unyanyasaji wa maelfu ya watu waliompinga kisiasa.
Tume ya ukweli iliyoundwa kuchunguza madai hayo ilipata ushahidi wa mauaji ya takriban watu 4,000 na ikakadiria kuwa huenda idadi hiyo ikawa mara 10 zaidi.
chanzo bbcswahili.com
Post A Comment
Hakuna maoni :