Muhuri, Haki Afrika zapinga kushirikiana na magaidi
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Muslims for
Human Rights (MUHURI) na HAKI AFRIKA yenye makao yao mjini Mombasa,
Kenya, yamesema kuwa serikali ya nchi hiyo inaendesha vita vya wazi
dhidi ya Waislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Tamko hilo la
mashirika hayo ni radiamali kwa hatua ya serikali ya kutangaza kuyapiga
marufuku mashirika hayo yasiyo ya kiserikali kwa tuhuma za kuwa na
mfungamano na makundi ya kigaidi. Mkuu wa Haki Afrika, Hussein Khalid na
mwenzake wa MUHURI, Khelef Khalifa wamesema mashirika yao yamepigwa
marufuku kutokana na kusimamia haki na ukweli na kuikosoa serikali kila
mara inapowakandamiza raia. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na
leo, viongozi wa mashirika hayo mawili wamesema ripoti zao za mara kwa
mara zinazoanika ukandamizaji wa polisi dhidi ya washukiwa wa ugaidi
ndizo zilizoikasirisha serikali na kusababisha mashirika yao kupigwa
marufuku. Wamesema hawaungi mkono ugaidi wala hawana uhusiano wowote na
makundi ya kigaidi lakini wametaka serikali kuwatendea haki washukiwa wa
ugaidi wanapokamatwa ili kudhihirisha kuwa Kenya ni nchi inayoheshimu
utawala wa sheria.
Post A Comment
Hakuna maoni :