
Bunge la Misri limeonyesha wasi wasi wake kutokana na kushadidi hali ya
ukandamizaji wa haki za binaadamu na kuzorota uchumi katika kipindi cha
miaka miwili iliyopita. Ripoti iliyoandaliwa na bunge la Misri kuhusiana
na hali ya haki za binaadamu na kadhalika hali ya uchumi wa nchi hiyo,
ilikusanywa tangu kulipojiri mapinduzi ya kijeshi dhidi ya aliyekuwa
rais wa taifa hilo Muhammad Mursi. Aidha ripoti hiyo imeelezea mauaji ya
zaidi ya watu 7,000 katika maandamano dhidi ya serikali, huku zaidi ya
watu elfu 50, wakiwamo wanaharakati wa kisiasa na haki za binaadamu
wapatao 236 wakiwa wametiwa mbaroni kwa makosa tofauti na polisi ya nchi
hiyo. Ripoti hiyo pia imeongeza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita, Misri imeshuhudia ukandamizaji wa kupindukia wa haki za
wanawake, watoto na wanafunzi huku mali za wapinzani 902, zikifilisiwa.
Aidha imeongeza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili hiyo, jumla ya
taasisi 1096, mashirika 532, shule 82 na hospitali na vituo vya afya 28,
vilisimamishwa na serikali ya Cairo. Kama hiyo haitoshi, serikali ya
nchi hiyo imekuwa ikitekeleza ukandamizaji wa kupindukia dhidi ya uhuru
wa kujieleza kwa kuzuia vyombo vya habari na mikusanyiko ya kisiasa. Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, wanahabari wasiopungua 10 waliuawa huku kanali
nne za televisheni zikifungwa. Aidha imeelezea kufungwa ofisi 12 za
upashaji habari, kuwaacha bila ajira wanahabari 30, kutiwa mbaroni
waandishi wengine wa habari wasiopungua 150 na kuripotiwa kesi 150 za
ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari.
chanzo(tehran radio idhaa ya kiswahili)
Post A Comment
Hakuna maoni :