Al Shabab waua askari 12 Wasomali, AU Somalia

Ripoti zinasema wanajeshi hao waliuawa katika hujuma ya bomu na mapigano yaliyofuatia siku ya Jumapili. Awali magaidi hao walilenga msafara wa kijeshi kwa bomu la kutegwa garini na kuwaua wanajeshi sita katika mji wa Manas katika eneo la Bay kusini mwa Somalia. Kufuatia hujuma hiyo mapignao yalijiri baina ya magaidi na wanajeshi hao ambapo wanajeshi sita waliuawa. Msemaji wa Jeshi la Somalia katika eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema magaidi 10 wa Al Shabab wameangamizwa katika mapigano hayo. Huku hayo yakijiri AMISOM imetangaza kuanzisha oparesheni mpya nchini Somalia kwa lengo la kuwatimua kikamilifu al Shabab katika maeneo ya kati na kusini mwa nchi hiyo. Kikosi cha AMISOM kina askari zaidi ya 20,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya Somalia kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab. Kikosi hicho cha AMISOM kinajumuisha askari kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya, na Sierra Leone. Al Shabab ambao pia wanatekeleza hujuma katika nchi jirani ya Kenya walianzisha vita dhidi ya serikali ya Somalia mwaka 2006.
(chanzo tehran radio idhaa ya kiswahil)
Post A Comment
Hakuna maoni :