
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa
limewatia mbaroni watu kadhaa katika jimbo la kaskazini mashariki la
Yobe ambao walikuwa wakisafirisha mafuta kuwapelekea wanamgambo wa kundi
la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram. Taarifa iliyotolewa na jeshi la
Nigeria imeeleza kuwa kufuatia maagizo yaliyotolewa kwa vikosi vya jeshi
hilo ya kuchunguza madereva na magari ya mizigo, askari wa divisheni ya
tatu ya jeshi wamewatia nguvuni baadhi ya vigogo na watu wanaowapatia
misaada magaidi wa Boko Haram na kuwanasa pia wakiwa na dawa za kulevya
na mada nyengine za kutia nishai. Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu hao
walikamatwa jana katika eneo lililoko baina ya miji ya Depchi na Gaidam,
kilomita 70 kusini mwa Damaturu, makao makuu ya jimbo la Yobe. Hata
hivyo taarifa hiyo haikueleza ni watu wangapi waliotiwa nguvuni katika
operesheni hiyo. Jana hiyohiyo pia jeshi la Nigeria lilipiga marufuku
utumiaji farasi katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno katika
jitihada za kukomesha mashambulio hatari ya kundi la kigaidi na
kitakfiri la Boko Haram. Msemaji wa Jeshi katika jimbo la Borno Kanali
Tukur Gusau amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kuzuia mashambulio ya
wanamgambo wa Boko Haram katika maeneo ya mbali katika jimbo hilo. Licha
ya hatua kadhaa zilizochukuliwa na Rais Muhammadu Buhari tangu
alipoingia madarakani mwishoni mwa mwezi wa Mei kwa lengo la
kulisambaratisha kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram,
mashambulio ya kundi hilo yangali yamepamba moto ambapo kwa mujibu wa
vyombo vya habari watu wasiopungua 1,000 wameuawa katika wimbi la
mashambulio yaliyofanywa na Boko Haram ndani ya muda wa chini ya miezi
mitatu…/
(tehranradio)
Post A Comment
Hakuna maoni :