
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Burundi imetangaza Rais Pierre
Nkurunziza kuwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika
Jumanne iliyopita. Tume ya uchaguzi imesema kuwa, Nkurunziza ameshinda
kiti cha urais baada ya kujipatia asilimia 65.41 za kura. Uchaguzi huo
ulifanyika Jumanne iliyopita licha ya kuweko malalamiko ya ndani na nje
na hata miito ya kutaka kuakhirishwa uchaguzi huo. Hata siku moja kabla
ya siku yenyewe ya kufanyika uchaguzi kulishuhudiwa matukio ya
ukandamizaji wa vyombo vya usalama dhidi ya wapinzani na watu kadhaa
kuuawa.
Nchi na taasisi nyingi duniani zilikataa kupeleka waangalizi kwenye
uchaguzi huo. Wapinzani walikuwa wakipinga hatua ya Nkurunziza kugombea
urais kwa mara ya tatu wakisema anaenda kinyume cha katiba na mapatano
ya amani ya mwaka 2006 ya mjini Arusha Tanzania.
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa vyama vyote nchini Burundi kuanza
mara moja mazungumzo ya kisiasa kwa ajili ya kutatua hitilafu zao na
kushughulikia changamoto zinazoikabili nchi hiyo.
(chanzo tehran radio)
Post A Comment
Hakuna maoni :