
Chama kikuu cha upinzani nchini Burundi kimetangaza rasmi kutoyatambua
matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo, ambayo yamempa ushindi Rais Pierre
Nkurunziza. Akiongea na waandishi wa habari Agathon Rwasa, Mkuu wa
chama cha FNL nchini Burundi amesisitiza kuwa, chama chake hakiyatambui
matokeo hayo ya uchaguzi wa tarehe 21. Rwasa ameutaja uchaguzi huo kuwa
uliokosa itibari na hivyo ametaka kuitishwa uchaguzi mkuu mpya ambao
utawashirikisha viongozi wa vyama vyote vya upinzani katika anga salama.
Aidha Agathon Rwasa amepinga pendekezo la kuunda serikali ya umoja wa
kitaifa, na kusisitiza kuwa, suala hilo litawezekana tu iwapo serikali
ya sasa itaandaa uchaguzi wa wazi na ulio huru na wa kidemokrasia
nchini. Licha ya kushadidi kwa wimbi la malalamiko ya ndani na nje
yaliyomtaka Rais Pierre Nkurunziza kuachana na azma yake ya kugombea
muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu, lakini rais huyo alipuuza
malalamiko hayo na kushiriki katika uchaguzi wa tarehe 21 mwezi huu
ambapo aliibuka kuwa mshindi. Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Rais
Nkurunziza ameshinda kwa kujizolea asilimia 69.41 ya kura zilizopigwa
huku Agathon Rwasa wa FNL akishikilia nafasi ya pili kwa asilimia 19 ya
kura hizo.
(chanzo tehran radio)
Post A Comment
Hakuna maoni :