Na sasa Marekani yakiri kuishambulia hospitali Afghanistan
Marekani imekiri kuwa iliishambulia hospitali katika hujuma yake ya hivi karibuni mjini Kunduz kaskazini mwa Afghanistan.
Meja Jenerali John Campbell, mkuu wa majeshi ya Marekani huko Afghanistan amedai mbele ya bunge la Marekani kuwa hospitali hiyo ililengwa 'kimakosa' siku ya Jumamosi. Katika shambulio hilo, raia 22 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Hospitali hiyo ilikuwa inasimamiwa na shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, Médecins Sans Frontières-MSF. Shirika hilo limesema wafanyakazi wake 12 waliuawa katika hujuma hiyo ya Marekani huku chumba cha kuwatibu wagonjwa mahututi (ICU) kikiharibiwa kabisa. MSF imelaani hatua ya jeshi la Marekani kuilenga hospitali hiyo na kusema hatua ya Washington kukiri kuilenga hospitali hiyo kwa mabomu ni sawa na kukiri kutenda jinai ya kivita. Marekani iliushambulia mji wa Kunduz baada ya wanagambo wa Taliban kuuteka mji huo. Kundi hilo la kigaidi bado linaendeleza harakati zake Afghanistan pamoja na kuwa Marekani na waitifaki wake waliivamia nchi hiyo mwaka 2001 kwa lengo la kuangamiza Taliban.
chanzo-tehran radio
Post A Comment
Hakuna maoni :