Tanzania yatishwa na ongezeko la wakimbizi wa Burundi

Wimbi la wakimbizi wa Burundi wanaoingia nchini Tanzania limeitisha serikali ya nchi hiyo na kuifanya ianze kuandaa mikakati ya kufungua kambi nyingine za wakimbizi. Ongezeko kubwa la wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma, limeifanya serikali ya Tanzania ifungue kambi nyingine tatu za Karago, Mtendeli na Nduta wilayani Kibondo ili kupunguza mlundikano wa wakimbizi katika kambi hiyo. Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Harrison Mseke amesema kuwa, kutokana na idadi ya wakimbizi kutoka Burundi kufikia 90,000 imekuwa vigumu kuwahudumia katika kambi moja kutokana na wingi wao. Harrison Mseke ameongeza kuwa, baada kushuhudia ongezekeko kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, serikali imeamua kuongeza kambi nyingine tatu ili iweze kuwahudumia vizuri. Taarifa zaidi zinasema kuwa, mpaka sasa kambi ya Nyarugusu ina wakimbizi laki moja na nusu (150,000) wakiwamo wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Burundi ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa tangu mwezi Aprili mwaka huu na zaidi ya raia laki moja wa taifa hilo wamekuwa wakimbizi katika nchi jirani za Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(tehran radio)
Labels
kimataifa
Post A Comment
Hakuna maoni :