Umoja wa Mataifa wataka utulivu uchaguzi wa Burundi

Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa mwito huo jana na kusisitiza kuwa, pande zote zitakazoshiriki kwenye uchaguzi huo wa leo, zinapaswa zijiepushe na fujo na machafuko.
Amesema, ana matumaini kufanyika uchaguzi huo kutairejesha Burundi kwenye utulivu na usalama.
Hii ni katika hali ambayo watu wasiopungua 100 wameuawa katika machafuko ya zaidi ya miezi miwili yaliyozuka nchini Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kugombea urais kwa kipindi cha tatu.
Uchaguzi wa rais unafanyika leo Jumanne nchini Burundi katika hali ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kushinda Rais Pierre Nkurunziza licha ya wananchi na wapinzani kupinga urais wake wa kipindi cha tatu mfululizo.
Wakati huo huo shirika la habari la AFP limeripoti kuwa uchaguzi huo unafanyika katika hali ambayo wimbi la wananchi wanaokimbia nchi hiyo kwa hofu ya kuzuka machafuko linazidi kuongezeka.
Katika upande mwengine Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) jana ilikataa ombi la kuitaka mahakama hiyo izuie kufanyika uchaguzi wa leo wa rais huko Burundi. Jopo la majaji watatu lililoongozwa na Bi Monica Muhenyi limetupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na Chama cha Mawakili cha Pan African (Palu) na Jukwaa la Taasisi za Kijamii za Afrika Mashariki.
chanzo tehran radio idhaa ya kiswahil
Post A Comment
Hakuna maoni :