Hatimaye shilingi ya Tanzania yaimarika sokoni

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya shilingi ya Tanzania kuanza kuimarika dhidi ya Dola, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya amezitaja mbinu zilizochukuliwa ili kuiimarisha ikiwa ni pamoja na kuzuia uhamishwaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine kitaalamu ‘swapping.’
Waziri Mkuya alisema uhamishaji huo utafanyika pale tu kutakapokuwa na shughuli za kiuchumi.
“Benki zilikuwa zinahamisha fedha kutoka benki
moja kwenda nyingine bila sababu za msingi za shughuli za kiuchumi, hii
ilisababisha kushuka kwa shilingi lakini kwa sasa tumezuia na itafanyika
pale tu gavana atakapoidhinisha,” alisema.
Waziri Mkuya alisema kwa muda mrefu Serikali
imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha shilingi inaimarika hivyo hayo
ndiyo matokeo yake. “Hii ndiyo hatua tuliyochukua, mlitusema vibaya
kwamba hatufanyi kazi lakini sisi tulikuwa tunachukua hatua kwa nafasi
yetu,” alisema.
Shilingi ya Tanzania ilianza kuimarika juzi, kwani
ilinunuliwa kati ya Sh1,700 na Sh1,900 badala ya Sh 2,400 ya awali
dhidi ya dola moja ya Marekani.
Wiki iliyopita, mporomoko huo ulizua mtikisiko wa
uchumi kiasi cha kuelezwa kuwa fedha hizo zingeweza kufikia kati ya
Sh2,500 na Sh2,800 wakati huo nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Akizungumzia jitihada zilizochukuliwa, Waziri
Mkuya alisema Serikali pia imepunguza uzuiaji wa dola kutoka asilimia 10
hadi nane ili kuipa nguvu shilingi.
“Serikali ilishika kiasi kikubwa cha fedha na sasa imepunguza asilimia 2, hiyo nayo imeleta unafuu,” alisema Waziri Mkuya.
Sababu nyingine ya kuimarika kwa shilingi
aliyoitaja Waziri Mkuya ni pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha
ambao ulikwamishwa kutokana na Bajeti ya Serikali na kusema kuwa kwa
sasa fedha nyingi zimeshaingia katika mifuko ya bajeti.
Kuanguka kwa shilingi kulitokana na uchumi wa
Marekani kukua jambo lililosababisha fedha za nchi nyingi kushuka ingawa
alisema shilingi ya Tanzania ilianguka zaidi.
Mkurugenzi wa Uchumi, Utafiti na Sera wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), Dk Joseph Massawe, alikaririwa na gazeti la The
Citizen juzi akisema kuwa shilingi imeimarika baada ya BoT kuingilia
kati tatizo lililojitokeza.
(chanzo mwanachi)
(chanzo mwanachi)
Post A Comment
Hakuna maoni :