Al-Shabab waua watu wasiopungua 25 Somalia
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa, kwa uchache watu 25 wameuawa baada
ya wanamgambo wanaofungamana na mtandao wa al-Qaeda wa al-Shabab kufanya
mashambulio mawili tofauti katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Abdulkadir Mohamed Nur Siidii Gavana wa jimbo la Lower Shabelle amesema
kuwa, kwa akali wanajeshi 15 na wanamgambo 10 wameuawa wakati kundi la
wanamgambo wa al-Shabab waliposhambulia majengo ya wanajeshi katika miji
ya Mubarak na Awdheegle.
Mashuhuda wanasema kuwa, mamia ya askari
wamepelekwa katika maeneo hayo kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo.
Sheikh Abdiasis Abu Muscab msemaji wa kundi la kigaidi la wanamgambo wa
al-Shabab amesema kuwa, wapiganaji wao ndio waliotekeleza shambulio
hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, askari wa kulinda amani wa Umoja
wa Afrika nchini Somalia, AMISOM wametangaza kuwa, wamefanikiwa
kufelisha shambulizi la kigaidi la wanamgambo wa ash-Shabab nchini humo.
Mmoja wa makamanda wa askari hao, amesema kuwa wanamgambo wa al- Shabab
walijaribu kudhibiti kambi za jeshi la serikali kusini mwa Somalia,
lakini askari wa AMISOM wakafanikiwa kuzima jaribio hilo
Post A Comment
Hakuna maoni :